Saturday, July 27, 2013

Gomesa Tv

Mchawi wa Bongo fleva ni Mbongo Fleva mwenyeweHuenda ukajiuliza  kwanini muziki wa Tanzania, hususani muziki wa kizazi kipya maarufu kama Bongo Fleva, ambao umeanza katika miaka ya tisini, lakini umeendelea  kusuasua katika ukuaji wake katika soko la kimataifa.
Mara nyingi wapenzi , wadau na wanamuziki wenyewe  wamekuwa wakiulizana  mchawi ni nani? Na wengine  kushikana uchawi wenyewe kwa wenyewe.
Lakini bado wakibaki na swali ni nani  anazuia muziki huu usifike mbali, na kubaki  kudumaa katika nchi za  Afrika Mashariki, huku wasanii wake wakipata umaarufu na fedha za muda mchache na  baadaye kupotea kama moshi wa sigara.
Hivi karibuni  mwandishi wa makala hii, kwa bahati  alifanikiwa kuiona moja ya video ya Tanzania inayoitwa Jikubali,  iliyoimbwa na msanii Ben Poul, ikionyeshwa kwenye  moja ya luninga  yenye nguvu kubwa Afrika na duniani yenye makazi yake huko Afrika Kusini ya  inayoitwa Channel O.
Hapo ndipo nilipoamua  kumtafuta msanii huyo na kumuuliza,  njia gani aliitumia na kufanikiwa  kupenya hadi wimbo wake kufika huko. Pia kutaka kujua ni  kwanini wasanii wengi wanashindwa kufikia hapo alipofikia yeye, inagawa wamekuwa wakifanya kazi nzuri na kujipatia umaarufu mkubwa.
Ingawa kwa mara ya kwanza mnamo miaka ya 2000,  video ya mwanamuziki  Judithi Wambura ‘Lady Jay Dee’ wimbo uliobeba albamu yake ya kwanza ‘Machozi’ uliwezwa kuonyesha.
Katika mika hiyo hiyo Kharid Mohamed ‘T.I.D’ na wimbo wake wa Tanzania Mie nao ukafanikiwa kutamba katika kituo hicho,  hata hivyo kwa muda wote huo hadi  leo hii video bado  zimekuwa zikisuasua kusogea mbele.
Ben Poul alianza kusema kwamba video yake, tofauti na video zingine ambazo zimekuwa zikipigwa katika kituo hicho cha luninga, ambazo zimekuwa zikighalimu zaidi ya milioni 10.
Anasema video hiyo, imemghalimu milioni 5 kuikamilisha lakini pia zilikuwa zikimtoka fedha zingine ndogo ndogo ambazo zilikuwa hazipo kwenye mahesabu. “Kikubwa sio ghalama kubwa ya kufanya video ndiyo ikaonyeshwa kamataifa, ila uzuri wa video na mazingira” anasema.
Anasema video yake aliifanya mkoani Arusha, chini ya mtayarishaji Nisher, ambaye kwa sasa anakuja kwa kasi.
Ban Poul anasema kabla ya kufanya video hiyo, alihakikisha anakamilisha kila kitu ilikuona anajituliza juu ya kazi yake.
Baada ya kuhakikisha amemaliza kazi zake zote, akahamishia nguvu zake kwenye video hiyo ambayo ilichukuwa wiki moja na nusu, kuikamilisha.
“Video inahitaji utulizaji wa akili, sio mtu unataka umalize kwa siku mbili, au tatu ili kukimbia bajeti.  Pia mtayarishaji sio anakuwa na haraka amalize ya kwako siku bili, akafanye ya mwingine, wote mnabidi mtulie” anasema.
Anasema katika video nzima ameonekana peke yake, ingawa ndani ya wimbo wenyewe alitaja majina ya wasanii, wanasiasa, na watu wengine zidi ya majina ishirini.
Lakini kutokana na mpangilio wa video hiyo, hakupaswa kuonekana mtu yoyote hata kwa bahati mbaya.
Walitumia wiki moja na nusu kuhakikisha wanapata picha za uhakika, na zenye mvuto na ndipo ikapatikana video hiyo ambayo ilianza kutikisa hapa nchini.
“Video ikawa imekamilika kwa mtindo huo, sikuwa na mtu yoyote katika video hiyo ambaye ningesema nilikuwa nae” anasema.
Kuhusiana na video yake kupigwa kwenye luninga ya Channel O, anasema  kwa mara ya kwanza alishawahi kupeleka video zake kwa mawakala wa Mtv Base na Channel O, waliokuwepo hapa nchini.
Video alizopeleka ilikuwa Maneno Maneno, na Samboila, lakini hazikuweza kufanya vizuri katika mchujo wa kuonyeshwa katika luninga hizo.
Lakini hakukata tamaa, alihakikisha kila siku anajitahidi kufanya vitu vingine zaidi mpaka akafanikiwa  kwa video yake ya jikubali kuonyeshwa.Hata hivyo anasema kinachopelekea video za Kitanzania, kuwa nyuma, ukitofautisha za Kenya, Ghana na Nigeria katika  kuonyeshwa kwenye luninga hizo, ni kutokuwepo kwa ushirikiano kwa wasanii wa Tanzania.
“Kila mtu anapanda kimafanikio kivyake, hakuna mtu ambaye anaweza kufanikiwa kwa kupitia mgongo wa mwenziwe. Lakini wanasahau hata kusaidiana” anasema.
Huenda hilo ndilo likawa tatizo kubwa, maana kila mtu anaanza hatua moja na sio mtu kuendeleza hatua ambazo mwenzake ameziacha.
Ben Poul anasema ukimfuata msanii mkubwa ambaye tayari video yake moja au mbili ilishaonyeshwa kwenye luninga hizo maarufu Afrika na Duniani, atakujibu kwamba video yake imeghalimu fedha nyingi sana kutengeneza,  au anaweza kukujibu kwamba amehonga ili kuicheza.
“Mtu ukimfuata kumuuliza juu ya kufanya vizuri kwa video yake, kwa lengo la kujifunza kupitia kwake anaweza kukukatisha tamaa kabisa” anasema.
Anasema hali hiyo imepelekea kuleta ugumu katika kuuliza, kwa maana hutopata jibu la uhakika. Hivyo anasema wasanii wengi wamekuwa wakianza hatua moja, na kila anayekuja amekuwa akianza hatua moja tena na wengi huishia njiani.
“Ilibidi hatua moja atakayovuka mmoja mwingine apate ushauri kutoka kwa yule, na hata kujua njia alizotumia ili asije akaanza mwanzo” anasema.
Anasema hadi video yake inafika pale ambapo imefika sasa hivi, ni juhudi zake mwenyewe bila ya kupata ushauri wowote zaidi ya kutuliza kichwa na kufanya kazi nzuri.
Lakini anasema kama kungekuwa na elimu nzuri, au ushirikiano baina ya wasanii wenyewe basi wasanii wengi wangeweza kufikisha mbali video zao.
Hiyo ndiyo miongoni mwa sababu kubwa ya kutosogea, au kusogea kwa kusua sua kwa muziki wa kizazi kipya katika soko la kimataifa ingawa, baadhi ya nyimbo zimekuwa zikifanya vizuri.
Miongoni mwa msanii ambaye niliwahi kumuuliza ni Emmanuel Rlibariki, ambaye yeye alisema wasanii hawapendani.
Anasema hawataki kumuona mtu anafanikiwa, hasa kupitia yeye anahitaji kila mtu kupambana mwenyewe.
“Mtu hataki kumuona msanii mwenzake anafanikiwa, wala kula chachu ya mafanikio ya mwenzake” anasema.
Huenda wasanii wasanii wengi wamesahau kwamba umoja ni nguvu, na utengano wao ndiyo sababu ya kuumia kwao kimaslahi na hata kimuziki kiasi cha kuonyeshana kidole, kumtamtafuta mchawi.
Mwisho.

Gomesa Tv

About Gomesa Tv -

Author Description here.. Nulla sagittis convallis. Curabitur consequat. Quisque metus enim, venenatis fermentum, mollis in, porta et, nibh. Duis vulputate elit in elit. Mauris dictum libero id justo.

Subscribe to this Blog via Email :

https://www.facebook.com/gomesamohamedi